Wafanyakazi wa utafutaji waliripoti kuwa hawakupata dalili zozote za uhai Jumatatu baada ya kufanikiwa kuiona helikopta iliyoanguka ikiwa imembeba Rais wa Iran Ebrahim Raisi na maafisa wengine wakuu kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.
Helikopta hiyo ilianguka Jumapili katika hali mbaya ya hewa karibu na Varzaqan katika mkoa wa Azerbaijan Mashariki wa Iran. Vyombo vya habari vya serikali vilisema kuwa helikopta hiyo ilikuwa ikimsafirisha Rais Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amirabdollahian na maafisa wengine wawili wakirejea Iran kutoka katika hafla mpakani katika mpaka na Azerbaijan, ambapo walikutana na Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev ili kuzindua mradi wa bwawa.
Vyombo vya habari vya Iran vilisema kuwa helikopta hiyo iliyoanguka ni moja ya helikopta tatu zilikuwa zikisafirisha maafisa wa Iran waliokuwa kutoka kwenye hafla hiyo, ambapo walizindua mitambo ya kuzalisha umeme ya Khoda Afarin na Giz Galasi kando ya Mto Aras alama ya mpaka kati ya Iran na Azerbaijan. Mitambo hiyo ipo kwenye ukingo wa mto kati ya wilaya ya Jabrayil Azerbaijani na mkoa wa Azabajani Mashariki wa Iran.