Vikosi vya Israel vilipambana na wanamgambo wa Hamas Jumanne huko Ukanda wa Gaza wakilenga zaidi kusini mwa Gaza huku mashirika ya kimataifa ya misaada yakielezea wasiwasi wao kwamba raia hawana njia salama ya kuondoka kutoka kwenye mzozo huo.
Vifaru na wanajeshi wa Israel walisogea karibu na Khan Younis, mji wa kusini ambao ni wa pili kwa ukubwa katika Ukanda wa Gaza, huku mashambulizi ya anga ya Israel yakipiga kusini mwa Gaza.
Maonyo kutoka kwenye jeshi la Israeli katika siku za hivi karibuni yaliwataka watu katika vitongoji vingi vya Khan Younis kuhama kwa usalama wao, na kuwaelekeza maeneo ya kusini zaidi.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu inasema takriban watu milioni 1.8 wamekimbia makazi yao ndani ya Gaza, wakati shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Kipalestina linasema karibu watu milioni 1 wanajihifadhi katika vituo vyake kusini mwa Gaza.