Sampuli ya pombe iliouwa Tanzania yachunguzwa na Mkemia Mkuu

Mtu aliyekunywa bonge ya kienyeji na kudhurika

Sampuli za vielelezo, ikiwamo ya miili ya watu waliofariki dunia Jumatano iliyopita baada ya kunywa pombe aina ya gongo kwa ajili ya uchunguzi ziko tayari kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa serikali nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari upelelezi wa awali umebaini kuwa, eneo la tukio kulikuwa kunauzwa pombe ya kienyeji na mtu mmoja aliyejulikana kama Mama Anoza.

Tatizo hili tayari limeathiri nchi nyingi za Afrika Mashariki ambapo watu wengi wamepoteza maisha au kuwa vipofu.

Vielelezo vyapelekwa kwa uchunguzi

“Vielelezo vyote pamoja na miili ya waliopoteza maisha vinapelekwa kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya uchunguzi ili tuweze kubaini chanzo halisi cha vifo hivyo,” amesema Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Lazaro Mambosasa.

Aliwataja waliofariki kuwa ni Maleo Ramadhani (45), Mohamed Issa (67), Kabugi Rashid (64), Stanslaus Joseph (58) wote wakiwa ni wakazi wa Kimara, Saranga.

“Wengine ni Stephen Isaya (61), Monica Rugaillukamu (42), Alex Madega (41), Hamis Mbala (35), Dikson Nyoni (28) pamoja na mtu aliyejulikana kwa jina moja la Yona, mwenye umri kati ya miaka 20 na 30.

Jeshi hilo bado linamtafuta Mama Anoza, aliyekuwa muuzaji wa pombe hiyo.

Uchambuzi wa wataalamu

Madaktari wameeleza kuwa sumu ya methanol inayopatikana ndani ya sprit ambayo inatajwa kama moja ya chanzo cha vifo vya watu zaidi ya 10 waliokunywa gongo, kwa kawaida sumu hiyo haihitajiki katika mwili wa binadamu.

“Mchanganyiko waliouweka hutengeneza vitu vingi ambavyo vina madhara makubwa kwa mwili wa binadamu zaidi kuliko pombe za kawaida ambazo tunazijua,” amesema Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ini na Mfumo wa Chakula wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Tuzo Lyuu.

“Lakini wakati mwingine ni katika hiyo ‘process’ ya kutengeneza hicho kinywaji… tunajua kuna temperature tofauti za utengenezaji na kukusanya zile product ambazo zinatengenezwa.

Alisema sumu hiyo ina madhara makubwa katika mwili wa binadamu, kwani huenda kuathiri moja kwa moja baadhi ya viungo, hasa macho na ubongo.