Maafisa wa usalama wa Somalia wanashuku kuwa kundi la Al Shabaab ndilo lilitungua ndege ya abiria na kusababisha kifo cha abiria mmoja mapema wiki hii.
Rubani wa ndege ya kampuni ya Daallo Airlines alilazimika kutua kwa dharura kwenye uwanja mmoja mjini Mogadishu baada ya mlipuko kutoboa shimo kando ya ndege hiyo dakika chache baada ya kupaa angani siku ya jumanne. Abiria 81 waliokuwa ndani ya ndege hiyo wamempongeza rubani huyo na wafanyakazi wa ndege kutokana na namna walivyokabiliana na ajali hiyo. Hakuna majeraha mengine yalioripotiwa wakati uchunguzi kutokana na tukio hilo ukiendelea.
Waziri wa anga na usafiri wa Somlia Ali Ahmed Jama aliiambia Sauti ya Amerika kwamba mwili wa mtu mmoja ulipatikana karibu na mji wa Bala’ad upo mikononi mwa wachunguzi.
Ahmed Elmi Muhamed afisa wa Somalia aliyekuwa kwenye ndege hiyo amesema kwamba wafanyakazi wa ndege hiyo mara moja walianza kuwatoa abiria waliokuwa karibu na sehemu iliyotoboka wakiwasaidia kuvaa vifaa vya kuvuta hewa kwa kutumia oxygen na kuwahakikishia kwamba watatua salama.