Uwanja wa ndege wa Istanbul wafunguliwa

Istanbul imefungua tena uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ataturk, baada ya shambulizi moja la kujitoa mhanga lililouwa watu 41 na kujeruhi zaidi ya 200 jana jioni.

Waziri Mkuu wa Uturuki, Binali Yildirim, alisema leo Jumatano kwamba uwanja wa ndege umefunguliwa tena kwa huduma za usafiri wa ndege.

Shirika la ndege la Uturuki (Turkish Airlines) linasema limeanza tena kufanya kazi kwa ndege zake zote na kwamba ndege kati ya Marekani na Istanbul zimeanza pia kufanya kazi.

Uwanja wa ndege wa Istanbul Ataturk

Kwa mujibu wa Gavana wa Istanbul, kiasi cha watu 10 waliofariki katika mashambulizi walikuwa raia wa kigeni na majeruhi 109 kati ya 239 wametolewa hospitalini leo Jumatano.

Wajitoa mhanga watatu wanaripotiwa kuwafyatulia risasi watu kadhaa kabla ya kutegua milipuko kwenye eneo la kuwasili abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Istanbul.