Utovu nidhamu kingono wagundulika ulikuwa wa kimfumo katika ligi ya wanawake Marekani

Wachezaji wa Washington Spirit wakishangilia baada ya kuwashinda Chicago Red Stars katika mechi ya soka ya Mashindano ya Wanawake -NWSL Jumamosi, Novemba 20, 2021, huko Louisville, Kentucky. (AP Photo/Jeff Dean).

Uchunguzi huru kuhusu kashfa zilizozuka katika Ligi ya Taifa ya Soka ya Wanawake ya Marekani uligundua unyanyasaji wa kihisia na utovu wa nidhamu wa kingono ulikuwa ni wa kimfumo katika mchezo huo, na kuathiri timu nyingi, makocha na wachezaji.

Shirikisho la soka la Marekani liliagiza uchunguzi ufanyike na aliyekuwa kaimu Mwanasheria Mkuu wa Marekani Sally Yates na kampuni ya wanasheria baada ya wachezaji wa zamani wa ligi ya wanawake Sinead Farrelly na Mana Shim kujitokeza na madai ya unyanyasaji na kulazimishwa kingono tangu miaka kumi iliyopita.

Lakini ilikuwa wazi matatizo yalikuwa yameenea. Makocha wakuu watano kati ya 10 kwenye ligi msimu uliopita walitimuliwa au kujiuzulu kutokana na madai ya utovu wa nidhamu.

Paul Riley, ambaye alikanusha kuhusika na madai hayo, alifukuzwa mara moja katika nafasi yake kama kocha mkuu wa North Carolina Courage, na Kamishna wa Ligi ya soka ya Wanawake Marekani-NWSL Lisa Baird akajiuzulu.