Akiwa katika Jumba lake la Kifahari Mar-a-Lago Club Florida ambapo atakuwepo wikiendi yote, rais anategemea kutumia muda wake Jumapili akiwasaili watu kadhaa ambao anataka mmoja wapo awe ni mshauri wa usalama wa taifa.
Trump amewaambia waandishi akiwa kwenye ndege ya Air Force One Jumamosi, “wengi sana wanataka kazi hiyo.”
Lakini Trump amesema “nimekuwa nikimfikiria mtu mmoja kwa siku tatu au nne, tutaona kile kitakacho tokea, nakutana na mtu huyo. Wote hao ni wenye uwezo, wote ni watu bora.”
Kati ya wale ambao wamepangiwa kukutana na Trump katika kusailiwa kuhusu nafasi hiyo ni anaye kaimu nafasi hiyo ya ushauri, mstaafu Luteni Jenerali Keith Kellogg; John Bolton, aliyekuwa balozi wa Marekani Umoja wa Mataifa; Luteni Jenerali wa Majeshi H R McMaster; na mkuu wa Chuo cha Kijeshi West Point, Luteni Jenerali Robert Caslen.
White House imesema kunaweza kukawa na mikutano mengine kuhusu kazi hiyo, ambayo imekuwa wazi wakati mstaafu Jenerali Michael Flynn alipoondolewa wiki iliyopita katika uongozi huo baada ya kutumikia kwa muda mfupi nafasi hiyo.
Trump pia amepanga kufanya mazungumzo ya simu na viongozi wa nchi nyingine na kuwa na mkutano wa sera ya huduma ya afya.
Wakati wa mkutano wake wenye staili ya kampeni Trump alisema uongozi wake umepiga “hatua ya ajabu” lakini akalalamika tena kile alichokiita utoaji habari zisizo za ukweli unaofanywa na vyombo vya habari vya Marekani.
Trump amerejea malalamiko yake aliyoyatoa White House juu ya waandishi kwa wakati alipozungumza nao siku ya Alhamisi kwa dakika 77.
Alisema vyombo vya habari vingi ni wazushi wa “habari feki” na kuwashutumu kuwa wanasema uongo kuhusu wanakozitoa habari hizo.
Halafu akaendelea kuwaambia watu waliokusanyika juu ya mambo mengi ambayo uongozi wake umefanya katika wiki nne tangu aapishwe.
“Niko hapa kuwajulisha hatua za ajabu tulizoweza kupiga katika kuifanya Marekani kuwa bora tena,” amesema. Nimekuja hapa kwa sababu nataka kuwa pamoja na marafiki zangu na wananchi.”
Jeshi la polisi Melbourne limesema takriban watu 9000 walihudhuria mkutano wa rais. Ndege ya Air Force One ilikuwa imeegeshwa karibu na mkutano.
Trump alikanusha habari kuwa wafanyakazi wa White House walikuwa hawana uwezo na wanakinzana. Alisema haya yote ni sehemu ya habari potofu.
Wakati anahutubia mara Trump alimwita kwenye jukwaa mmoja wa wafuasi wake aliyekuwa anazuiliwa na watu wa usalama akijaribu kusogea karibu na rais, naye akawaambia wamwachie aje mbele.
Rais alimpa nafasi ya kuelezea jinsi anavyo muunga mkono. Sidhani watu wa usalama waliona hilo ni jambo zuri, mtu huyo kunikaribia. Lakini akanong’ona kwa baadhi ya watu jukwaani sisi tunawajua watu wetu.”