Utawala wa Sudan waahidi ushirikiano katika uchunguzi wa uhalifu wa kivita Darfour-ICC

Mkuu wa jeshi la Sudan na kiongozi wa baraza kuu Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, Oktoba 26,2021. Picha ya AFP

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu (ICC) amesema Sudan imeahidi kutoa ushirikiano kamili katika uchunguzi wa uhalifu wa kivita na ukatili uliotekelezwa katika jimbo la Darfur chini ya uongozi wa rais aliyeondolewa madarakani Omar al-Bashir.

Karim Khan alizungumza hayo baada ya kukutana na mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan, ambaye alichukua madaraka mwaka jana katika mapinduzi, na ilikuwa baada ya kutembelea kambi huko Darfur, ambako Umoja wa mataifa unasema watu 300,000 waliuawa wakati wa mzozo ulioanza mwaka 2003.

“Maneno ambayo nimesikia kutoka kwa mwenyekiti wa baraza kuu ni mazuri sana,” Khan, ambaye alikuwa katika taifa hilo tangu Jumamosi, aliwaambia waandishi wa habari.

“Changamoto sasa ni kuweka maneno hayo katika vitendo.”

Bashir, mwenye umri wa miaka 78, ambaye amefungwa jela mjini Khartoum tangu kuondolewa madarakani mwaka 2019, amekuwa akisakwa na ICC kwa zaidi ya muongo mmoja kwa mashtaka ya mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu huko Darfur.

Wasaidizi wake wawili wa zamani wanasakwa pia na mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague kujibu mashtaka ya uhalifu wa kivita.