Utapiamlo waongezeka kwenye kambi za wakimbizi kaskazini mwa Kenya

Picha ya anagani ya sehemu ya kambi ya wakimbizi ya Daadab, kaskazini mwa Kenya.

Shirika moja la kutetea haki za binadamu limeelezea wasi wasi wake kutokana na kuongezeka wa utapiamlo kwenye kambi za wakimbizi kasakazini mwa Kenya.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, International Rescue Committee, limesema Alhamisi kwamba watoto wameathiriwa zaidi, wakati viwango vya chakula vikishuka kutokana na kupungua kwa misaada.

Shirika hilo limeongeza kusema kwamba idadi ya wagonjwa waliolazwa hospitalini kutokana na utapiamlo imeongezeka kwa karibu asilimia 95 mwezi Mei, ikilinganishwa na mwezi uliotangulia kwenye kambi ya wakimbizi ya Hagadera ndani ya ile kubwa ya Daadab, ambayo kwa kawaida hutoa hifadhi kwa wakimbizi kutoka Somalia.

Wakimbizi wengine kutoka Sudan Kusini, Uganda na Burundi wanaoishi kwenye kambi ya Kakuma pia wanasemekana kuathiriwa vibaya. Kenya inatoa hifadhi kwa zaidi ya wakimbizi 600,000, kwenye kambi za Daadab na Kakuma, pamoja na kwenye miji midogo.

Ukanda wa Afrika Mashariki unakumbwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kutokea katika miongo kadhaa kufuatia kukosekana kwa mvua kwa misimu sita mfululizo.