Usalama wa Taifa wakabiliwa na shutma za utekaji nyara

Bunge la Tanzania

Bunge la Tanzania limepewa taarifa juu ya madai ya kuwa kuna kikundi ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa ambacho kimeamua kuchukua mamlaka yakuteka watu, jambo ambalo limekuwa linaharibu heshima ya serikali na Chama cha Mapinduzi.

Wabunge wawili wameomba kuwa shughuli za bunge ziahirishwe ilikujadili suala la dharura ambalo limehusisha watu kutekwa nyara.

“Naomba mheshimiwa naibu spika tulijadili suala hili kama bunge na ikikupendeza bunge hili liunde kamati maalumu yakuweza kuchunguza jambo hili linaloendelea katika nchi yetu,” amesema Hussein Bashe.

Bashe (CCM) ameliambia bunge kwamba baadhi ya mawaziri wamemtahadharisha kuwa makini kwani yeye ni mmoja kati ya wabunge 11 ambao wako katika orodha, wakisema mkikaa barabarani vibaya mnaweza kupoteza maisha yenu.

Bashe alisema iwapo kuahirisha hakutowezekana basi spika aiagize kamati ya bunge ya kudumu ya mambo ya nje, ulinzi na usalama iweze kufanya kazi yake na kumletea taarifa kwa ajili ya usalama wa wananchi wa nchi hii.

“Hali ya nchi sio salama, watanzania wanataharuki, watanzania wanajadili mambo haya katika mitandao,” alisisitiza Bashe.

“Hakuna tamko lolote la serikali linaleta matumaini,” aliongeza.

Akiwasilisha maombi yake kwenye bunge hilo Bashe amesema kuwa miongoni mwa watu waliowahi kutekwa ni Joseph Msukuma, Bashe (wakati wa mkutano mkuu wa CCM), Adam Malima, na Ben Saanane ambaye amepotea mpaka hivi sasa.

Akizungumza kwa huzuni kubwa Bashe amesema kuwa juzi tu Roma Mkatoliki alitekwa.

“Mheshimiwa Naibu spika nasema ni jambo la dharura kwa sababu hawa ni wale wanaofahamika. Hatujui ni watanzania wangapi hawafahamiki katika ngazi za chini.

Kwa upande wake Mbunge Joseph Mbilinyi (Chadema) alitoa hoja kama ya Bashe, akinukuu kanuni ya 47 juu ya kuahirishwa shughuli za bunge ilikujadili suala la dharura la kutekwa watu nchini.

Mbilinyi alisema kumekuwa na utamaduni ambao sio wa kawaida wa kimafia wa kuteka watu nyara.

“Tokea operesheni hii ya kuteka watu ianze kila anayehusika na usalama, likiwemo jeshi la polisi anasema hatujui, hatujaona kwenye vituo vyovyote, na nchi inabaki kwenye taharuki,” amesema mbunge huyo.

Akielezea matukio makubwa nchini Mbilinyi ametaja kupotea kwa Bensanane, mara miili sita, saba imeokotwa mto ruvu na ikaende kuzikwa bila ya kufanyiwa postmortem kwa amri ambayo hatujui ni ya nani.

Mbunge huyo alisema: “Bashe alitekwa, Nape alitekwa na akaokolewa na Maulid Kitenge, vinginevyo angekuwa ametekwa, lakini hakuna mtu aliyezungumza kitu. Waziri wa Mambo ya Ndani yupo kimya mpaka najiuliza kama anabanwa kwa kiasi hicho.”

Mbilinyi ameongeza kusema: Huyu ni mtu mwenye uwezo ambaye alifikia daraja la kugombea urais, na bado anamustakbali, kwa nini asijiuzulu alinde heshima yake badala ya kukaa kimya katika vurugu hii.”

Akijibu ombi la wabunge hao, Naibu Spika wa Bunge, Dr Tulia Ackson amesema kuwa suala hilo lililotajwa sio la dharura.

“Sitalihesabu ya kwamba ni jambo la dharura lakini ni jambo ambalo utaratibu wa kawaida wa sheria unaweza ukafanya kazi,” alifafanua.

Aliongeza kusema kuwa jambo lolote litahisabiwa ni lenye maslahi ya umma iwapo utatuzi wake unategemea hatua zaidi kuliko zile za utekelezaji wa kawaida wa kisheria peke yake.

“Waheshimiwa wabunge masuala haya yalioulizwa na Bashe na Mbilinyi yako chini ya utaratibu wa Kisheria,” alisema.

“Bunge hili litashughulika na mambo ambayo yenye maslahi ambayo sheria haina uwezo wa kutolea majibu,”aloingeza.