Kituo cha uratibu kinachoongozwa na Umoja wa Mataifa kimesema kwamba meli hizo zimeondoka Ukraine kwa kuzingatia makubaliano kati ya serikali ya Ukraine, Uturuki na Umoja wa Mataifa, na kwamba Russia imepewa taarifa kuhusu usafiri wake.
Makubaliano ya kusafirisha chakula kutoka bandari za Ukraine, yalipatikana kufuatia mazungumzo yaliyosimamiwa na Uturuki na Umoja wa Mataifa mwezi Julai.
Russia ilikuwa imezuia usafirishaji wa nafaka na ngano kutoka Ukraine na kupelekea uhaba mkubwa wa bidhaa hizo katika soko la kimataifa.
Meli 12 ziliondoka Ukraine Jumatatu.
Rais wa Russia Vladimir Putin amesema kwamba hatua ya Russia ya kujiondoa katika makubaliano hayo inatokana na shambulizi la ndege zisizokuwa na rubani dhidi ya meli za Russia huko Crimea, lililotokea Jumamosi. Russia imedai kwamba Ukraine ndio ilitekeleza shambulizi hilo.
Ukraine haijasema iwapo ilihusika na shambulizi hilo na imefutilia mbali madai ya kutumia njia ya kusafirisha nafaka iliyokubaliwa katika mkataba, kwa sababu za kijeshi.
Waziri wa ulinzi wa Uturuki Hulusi Akar, amemwambia waziri wa ulinzi wa Ukraine kwamba kuendelea kutekeleza makubaliano ya kusafirisha nafaka na ngano ni muhimu sana, na kwamba mpango wa kibinadamu unastahili kuheshimiwa katika vita vya Ukraine.