Mwakilishi maalum wa Marekani kwa Sudan, Scott Gration, anasafiri kuelekea Khartoum kuzungumzia utekelezaji wa mkataba wa amani wa mwaka 2005, ambao ulimaliza miongo ya vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hiyo ya Afrika.
Mkataba unatoa wito wa kuitishwa kura ya maoni juu ya uhuru wa Sudan kusini mwezi ujao. Gration anatarajiwa kukutana na maafisa waandamizi wa Sudan na kuwasihi kuwa kura ya maoni ifanyike kama ilivyopangwa.
Mwakilishi huyo pia atatembelea Sudan magharibi katika mkoa wa Darfur, na kwa muda wa siku tatu atakutana na maafisa wa tume ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika-UNAMID, kuzungumzia usalama na hali ya kibinadamu huko.
Safari ya Gration inaishia Qatar kwa mazungumzo na maafisa wa serikali ya Qatar pamoja na wale kutoka Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika juu ya njia za kurahisisha mazungumzo ya amani yanayoendelea yanayojumuisha vyama katika mgogoro wa Darfur.