Marekani yaondoka rasmi Iraq

  • Mkamiti Kibayasi

Bendera ya Marekani, bendera ya Iraq na rangi za bendera za wanajeshi wa nchi hizo mbili zikipeperushwa wakati wa sherehe hiyo muhimu huko Baghdad, Disemba 15, 2011

Marekani yakamilisha kumalizika kwa kazi zake nchini Iraq kwa sherehe zilizohudhuriwa na Waziri wa ulinzi wa Marekani huko Baghdad

Waziri wa ulinzi wa Marekani, Leon Panetta anasema ndoto ya uhuru na ukombozi nchini Irak sasa ni ya kweli, wakati Marekani inakamilisha mwisho wa kazi zake za kijeshi nchini Irak.

Panetta alizungumza Alhamis kwenye sherehe huko Baghdad, akisema kuwa ni “tukio la kihistoria” kwa watu wote wa Irak na Marekani. Ikiwa ni wiki kadhaa kabla ya kufika Disemba 31, tarehe ya mwisho ya wanajeshi wa Marekani kuondoka nchini Irak. Kulikuwa na wanajeshi 4,000 wa Marekani waliobaki nchini Irak hapo Alhamis, ambapo idadi imeshuka kutoka wanajeshi 170,000 waliokuwapo wakati wa kilele cha vita.

Panetta alisema wanajeshi hao wataondoka Iraq wakijua kwamba waliwasaidia watu wa Irak kuanza ukurasa mpya katika historia yao ambayo ni “huru kutoka udiktekta” na matumaini makubwa ya mafanikio na amani.

Alisema kwamba “umwagikaji mkubwa wa damu umetokea” kwa watu wote wa Marekani na Iraq. “Lakini maisha hayo hayajapotea katika mishipa yetu. Wameleta uhuru na ukombozi wa Iraq. Na kwa sababu ya mihangaiko waliyoyapata, miaka hii ya vita imetoka hadi kuingia kwenye enzi mpya ya matumaini. Kwa pamoja na watu wa Iraq, Marekani inakaribisha hatua nyingine ya uhusiano wa Marekani na Iraq, hatua moja ambayo itaanzisha maslahi ya pamoja na heshima”.

Takribani wanajeshi 4,500 wa Marekani na maelfu yaw a-Iraq wameuwawa tangu vita vilipoanza mwezi Machi mwaka 2003.

Tarehe za matukio muhimu katika vita vya Iraq

Machi 20, 2003: Majeshi ya Marekani yaliivamia Irak.

April 9, 2003: Majeshi ya Marekani yaiingia Baghdad.

Mei 1, 2003: Rais George W.Bush anasema operesheni kubwa ya mapambano imeisha nchini Irak.

Disemba 13, 2003: Saddam Hussein akamatwa karibu na eneo alikozaliwa la Tikrit, kaskazini ya Baghdad.

Disemba 30, 2006: Saddam anyongwa.

Januari 10, 2007: Rais Bush atangaza kuongezwa zaidi ya wanajeshi 21,000 kupambana na ghasia zinazoongezeka.

Julai 22, 2008: Operesheni ya wanajeshi yasitishwa na kuacha kiasi cha wanajeshi 147,000 wa Marekani nchini Iraq.

Novemba 27, 2008: Bunge la Marekani laidhinisha mkataba wa usalama kati ya Marekani na Irak, ambao ulipanga tarehe ya Disemba 31, 2011 kwa majeshi yote ya Marekani kuondoka nchini Iraq.

Februari 27, 2009: Rais Barack Obama asema wanajeshi wote isipokuwa 50,000 wataondoka ifikapo Agosti 31, 2010.

June 30, 2009: Wanajeshi wa Marekani wanaondoka katika miji ya Iraq na kukabidhi majukumu ya usalama kwa majeshi ya Iraq.

Agosti 31, 2010: Rais Obama atangaza mwisho wa kazi za wanajeshi wa Marekani nchini Iraq. Kiasi cha wanajeshi 50,000 wanabaki ili kutoa mafunzo na ushauri kwa majeshi ya Iraq.

Disemba 21, 2010: Baada ya ucheleweshwaji wa miezi tisa, Iraq yaikubali serikali mpya.

Agosti 2, 2011: Viongozi wa kisiasa nchini Iraq wakubali kuzungumza uwezekano wa mkataba ambao utaruhusu baadhi ya wanajeshi wa Marekani kuendelee kuwepo nchini humo baada ya kazi za kutoa mafunzo kumalizika mwezi Disemba.

Agosti 15, 2011: Mashambulizi ya mabomu katika miji 17 nchini Iraq na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 60, na kuongeza wasi wasi kuhusu usalama baada ya majeshi ya Marekani kuondoka.

Septemba 1,2011: Jeshi la Marekani lasema hakuna mfanyakazi yeyote wa Marekani aliyekufa nchini Iraq mwezi Agosti, ambapo ni mwezi wa kwanza bila kutokea janga la vifo kwa jeshi la Marekani.

Octoba 21, 2011: Rais Obama athibitisha wanajeshi wote wa Marekani wataondoka nchini Iraq mwishoni mwa mwaka huu.

Novemba 29, 2011: Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden awaambia viongozi wa Iraq kuwa nchi hizi mbili zinaingia kwenye “hatua mpya” wakati Marekani inakaribia kumaliza kuondoa wanajeshi wake huko.

Disemba 14, 2011: Siku kadhaa baada ya mkutano na Waziri Mkuu wa Iraq, Nouri al-Maliki, Rais Obama asema wanajeshi wa Marekani wanaondoka wakiiacha Iraq huru, thabiti na ina uwezo wa kujiendesha yenyewe.

Disemba 15, 2011: Waziri wa ulinzi wa Marekani Leon Panetta asafiri kuelekea Baghdad kwa sherehe za maadhimisho ya kumalizika kwa kazi za Marekani nchini Iraq.