Marekani yatoa wito wa mkataba wa mafuta kabla kura ya maoni Sudan

  • Mwandishi Wetu

Mjumbe maalum wa Marekani huko Sudan Scott Gration.

Mjumbe maalum wa Marekani Sudan asema mkataba wa mafuta ni muhimu kabla ya kura ya maoni nchini Sudan.

Mjumbe maalum wa Rais Barack Obama kwa ajili ya Sudan, Scott Gration, anasema anaamini kuwa mkataba wa mafuta unahitajika kuwepo kabla ya kufanyika kwa kura ya maoni juu ya uhuru wa Kusini Januari 2011.

Kura hiyo ni sehemu muhimu ya makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka 2005, ili kumaliza miongo kadhaa ya mizozo baina ya Kusini na Kaskazini Sudan. Bwana Gration anasema ni muhimu kwa serikali ya Khartoum na utawala wa Sudan Kusini, kukubaliana juu ya jinsi ya kugawana raslimali ya mafuta, huku ikiwa inafahamika kuwa mafuta mengi zaidi yapo huko Kusini na miundo mbinu iko huko Kaskazini.

Alisema hayo jumanne jioni katika taasisi ya mikakati ya kimataifa mjini Washington, mbele ya dazeni kadhaa za watu mashuhuri, wasomi, na wafanyakazi wa kutowa misaada.

“Hii itabidi ijadiliwe kwa sababu pande zote zinahitaji mapato ya kigeni, lakini, pili, sidhani kutakuwa na kura ya maoni hadi pale suala hili litakapotatuliwa," alisema.

Alisema na lazima kuwe na ushindi pande zote, kuweza kunufaika kutokana na utajiri wa mafuta. Bwana Gration alikiri kuwa kuna changamoto nyingi zinazokabili utaratibu wa kura ya maoni, hususan eneo lenye utajiri wa mafuta la Abyei. Eneo hilo linalogombaniwa liko mpakani baina ya Kusini na Kaskazini, linatarajiwa kufanya kura yake tofauti, juu ya hali yake ya baadaye.