Upinzani Kenya waunda kamati ya kitaifa ya "bunge la wananchi"

Kiongozi wa upinzani Kenya, Raila Odinga awahutubia wafuasi wake mjini Nairobi, Kenya, Nov. 28, 2017.

Muungano wa upinzani nchini Kenya, NASA, Ijumaa ulizindua kamati ya kitaifa ya kuratibu mikakati ya kuunda "bunge la wananchi."

Kamati hiyo ya wanachama sita imetwikwa jukumu la kuongoza na kutoa ushauri kwa mchakato ambao, NASA imesema, utapelekea mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi nchini humo.

Taarifa iliyosomwa na aliyekuwa gavana wa Bungoma Bonnie Khalwale mjini Nairobi, ilisema kuwa kamati hiyo itaongozwa na mchumi David Ndii, ambaye ni mshauri mkuu wa muungano huo.

"Kamati hiyo itawasilisha ripoti yake kwa vinara wa muungano wa NASA kabla ya Desemba 12," alisema Khalwale.

Aliyekuwa mgombea urais kwa tikiti ya muungano huo, Raila Odinga, alisema mapema wiki hii kwamba "ataapishwa' tarehe 12 Desemba kama 'rais wa wananchi.'

Khalwale alisema kamati hiyo aidha itatoa ratiba ya mkutano wa kumuapisha Odinga.

NASA imesema baadhi ya kaunti zitaendelea kujadili mswada wa bunge la wananchi licha ya mahakama moja mjini Kitui kuamuru usitishwaji wa mjadala kuhusu mswada huo.

Miswada hiyo tayari imejadiliwa na kupitishwa katika kaunti za Kisumu, Homa Bay, Siaya, Busia, Kakamega, Vihiga, Kituai, Kwale, Makueni na Migori, ambazo ni ngome za upinzani.

Odinga alijiondoa kama mgombea wa urais kwenye uchaguzi wa marudio uliofanyika Oktoba 26 kwa madai kwamba usingekuwa huru na wa haki.

Uchaguzi huo ulikuwa umeitishwa na tume ya IEBC kufuatia uamuzi wa mahakama wa kubatilisha uchaguzi wa awali uliofanyika tarehe nane mwezi Agosti, kwa kile jaji mkuu alikieleza kuwa "kugubikwa na dosari na uvunjifu wa sheria."

Rais Uhuru Kenyatta aliapishwa kwa muhula wa pili tarehe 28 mwezi Novemba baada ya ushindi wake kuhalalishwa na mahakama ya juu.