UNICEF: Takriban watoto 1,000 wameuawa tangu Russia iivamie Ukraine

Picha inaonyesha eneo la karibu na jengo la utawala wa jimbo, ambalo maafisa wanasema lilishambuliwa na kombora, katikati mwa Kyiv, Machi 1, 2022. Picha ya Reuters

Shirika la Umoja wa mataifa linalohudumia watoto (UNICEF) linasema takriban watoto 1,000 wa Ukraine wamethibitishwa kuuawa au kujeruhiwa tangu Russia iivamie Ukrainie miezi sita iliyopita.

UNICEF imesema Jumatatu kwamba hesabu yake ya jumla ya watoto 972 waliouawa inajumuisha wale tu ambao wamethibitishwa na Umoja wa mataifa na kusema idadi ya kweli huenda ikawa kubwa zaidi.

Vifo vingi vya watoto hao vilisababishwa na silaha za milipuko, kulingana na taarifa ya mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Catherine Russell.

“Kwa mara nyingine, kama katika vita vyote, maamuzi ya kutojali ya watu wazima yanaweka watoto katika hatari kubwa. Hakuna operesheni za kutumia silaha za aina hiyo ambazo hazisababishi watoto kudhuriwa,” Russell ameandika.

Russel amesema mbali ya watoto waliouawa au kujeruhiwa katika machafuko hayo, “karibu kila mtoto nchini Ukraine amekabiliwa na matukio yenye kuhuzunisha sana, na wale wanaokimbia machafuko wako katika hatari kubwa ya kutengana na familia, machafuko, unyanyasaji, kudhulumiwa kingono, na usafirishaji haramu.”

Russell anasema shirika lake linakadiria kuwa shule moja kati ya 10 nchini Ukraine ziliharibiwa au kubomolewa katika vita.

UNICEF imetoa wito wa kumaliza matumizi ya silaha za milipuko katika maeneo yanayokaliwa na watu wengi, vile vile mashambulizi dhidi ya majengo ya raia na miundombinu.