Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto, UNICEF, Alhamisi alisema kwamba Watoto milioni 16 nchini Sudan wanateseka vibaya kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Alisema wengi wao wanakabiliwa na vitisho vya ukatili vya kila siku, njaa, magonjwa na unyanyasaji wa kingono.
“Mapigano yanafanyika mbele ya milango yao, karibu na nyumba zao, shule zao na hospitali, na katika miji mingi na vijiji vya Sudan,” Catherine Russell, mkurugenzi mtendaji wa UNICEF, aliuambia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Amesema Watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano wako hatarini zaidi, ambapo zaidi ya milioni 1.3 wanaishi katika maeneo matano yanayokabiliwa na njaa nchini humo, na wengine milioni 3 wako katika hatari ya magonjwa ikiwemo kipindupindu, malaria na homa ya dengu kutokana na kudorora kwa mfumo wa afya.
Takriban vijana milioni 16.5 hawako shuleni.