UNHCR yaziomba nchi jirani za Sudan kufungua mipaka kwa wanaokimbia mapigano

Watu wakikimbia mapigano kusini mwa mji mkuu Khartoum, Aprili 18, 2023

Shirika la Umoja wa mataifa linalohudumia wakimbizi (UNHCR) linatoa wito kwa nchi jirani za Sudan kufungua mipaka yao kwa ajili ya watu wanaokimbia mapigano ambayo yalizuka tarehe 15 Aprili.

Tangu mapigano kuzuka kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) Aprili 15, maelfu ya Wasudan wamelazimika kuhama makazi yao.

Kamishna mkuu wa UNHCR Filippo Grandi amerejelea wito uliotolewa mara kwa mara na katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres kutaka mapigano yasitishwe mara moja na kwa pande zote zianze juhudi za kuleta amani.

“Hii inahitajika pia kwa haraka ili kuzuia mzozo mwingine mkubwa wa wakimbizi ambao unaweza kuyumbisha zaidi usalama wa eneo dhaifu,” Grandi amesema katikka taarifa.

Licha ya pande zinazozana kukukabili kuongeza muda wa sitisho la mapigano, mapigano yaliripotiwa Alhamisi mjini Khartoum na katika jimbo la magharibi la Darfur.