UNHCR yaripoti ukame nchini Somalia unasababisha mzozo wa kibinadamu na ukosefu wa makazi.

Jumuiya ya Afrika mashariki yatoa wito kusaidia janga njaa na ukame Somalia.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) linaripoti ukame nchini Somalia unasababisha mzozo wa kibinadamu na ukosefu wa makazi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) linaripoti ukame nchini Somalia unasababisha mzozo wa kibinadamu na ukosefu wa makazi.

UNHCR inasema maelfu ya watu wanakimbia maeneo yenye ukame wakitafuta ardhi yenye rutuba na misaada ya kibinadamu ili kuweza kujinusuru kimaisha.

Nchini Somalia, watalaamu wanasema mabadiliko ya hali ya hewa yanaingia kwa kasi kubwa. Kwa muda wa miaka mitatu iliyopita, mvua kwa kiasi kikubwa zimeshindwa kunyesha, na kuangamiza mazao na mifugo.

UNHCR inaripoti kuwa maelfu ya watu wamekimbia makazi yao wakitafuta ardhi za malisho kwa ng’ombe wao na chakula, makazi na maji salama ya kunywa.

Shirika la kuhudumia wakimbizi linakadiria kuwa watu nusu milioni mwaka huu pekee watakosehwa ifikapo mwisho wa mwezi Machi. Wengi wao wameripotiwa ni watoto, wazee, waja wazito na kina mama wanaonyonyesha.

Msemaji wa UNHCR Boris Chershirkov anasema wengi wanawasili katika vituo vya mijini au kwenye makazi yaliyopo kwa ajili ya watu wasiokuwa na makazi na kukuta hali ngumu ya kimaisha. Ukiongezea, anasema matumaini ya misaada nayo yana upungufu na kuwalazimisha watu kubuni njia mbali mbali za kijikimu. Hili, anasema linawaweka katika hali ya kunyonywa na hatari mbali mbali.

“Watoto wameacha shule ili kuzisaidia familia zao kujipatia mapato ya kila siku na kutafuta maji na ardhi za malisho ya mifugo. Hii imewafanya kuwa katika mazingira hatarishi kama vile kulazimishwa kuolewa, familia kutengana, na manyanyaso ya ngono na mengine. Wanawake na wasichana, ni nusu ya watu wasiokuwa na makazi, na wako katika hatari kubwa sana,” Chershikov anasema.

Watabiri wa hali ya hewa wanasema kutakuwa na msimu mzuri wa mvua katika Pembe ya Afrika. Hivi sasa, msemaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani Tomson Phiri anasema hakuna eneo ambalo limeripotiwa ama kuwa katika hali ya njaa au linakaribia kukumbwa na njaa.

“Hata hivyo, njaa na utapiamlo vinazidi kuwa katika hali mbaya sana kote katika maeneo yaliyokumbwa na ukame. Msimu mmoja wa mvua huenda usitoshe kuondoa misimu mitatu ya ukame. Na kama misaada ya haraka ya kibinadamu haitapatikana, hali inaweza kubadilika haraka sana, na mamilioni ya familia huenda yakajikuta yakikabiliwa na njaa,” Phiri anasema.

Mashirika ya misaada yanakabiliwa na hali ya njaa kama iliyokuwa mwaka 2011 nchini Somalia, ambapo zaidi ya watu robo milioni wengi wao watoto walifariki.

UNHCR imeomba takriban dola milioni 157.5 ili kugawa misaada muhimu na kuwalinda takriban watu milioni tatu waliokoseshwa makazi ndani ya Somalia, na maelfu ya wakimbizi na wale wanaotafuta hifadhi. Hadi hivi sasa, ni asilimia tano tu ya kiwango hicho kimepokelewa.