Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema linawasiwasi na sehemu za mapendekezo ya Umoja wa Ulaya na Uturuki ya kukabiliana na mmiminiko wa wakimbizi na wahamiaji nchini Ugiriki.
UNHCR imesema kwamba mapendekezo hayo yaweza kuvunja sheria ya kimataifa.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa liemesema baadhi ya sehemu za mapendekezo ya makubaliano baina ya viongozi wa Umoja wa Ulaya na Uturuki zinahitaji kufafanuliwa.
Lakini UNHCR imesema inapata wasiwasi kuhusu mipango yoyote ambayo inahusisha kurudishwa kwa watu wote kutoka nchi moja mpaka nyingine.
Umoja wa Ulaya na Uturuki wamekubaliana kurudisha wahamiaji wote wanaowasili kutoka Ugiriki wakitokea Uturuki.
Mratibu wa UNHCR kwa upande wa Ulaya, Vincent Cochetel, amesema hafahamu yaliyomo kwenye mpango huo, lakini ana wasiwasi kwamba yanaweza kuwa hayana mashauri ya kuwalinda wale wanaotafuta hifadhi.
Mnamo mwaka jana, zaidi ya wakimbizi milioni moja na wahamiaji walichukua uamuzi wa hatari kusafiri kupitia bahari ya Mediterranean kutokea Uturuki kwenda Ulaya. Wengi wao waliwasili nchini Ugiriki.
Kikosi cha ulinzi wa mwambao wa Uturuki kimeripotiwa kuwazuia wale wanaodhaniwa kuwa ni wahamiaji wasio wa ikiwa ni juhudi za kuzuia usafirishaji wa binadamu.
Mratibu huyo, Cochetel ameiambia VOA kwamba hana pingamizi lolote na uzuiaji huo katika himaya ya bahari ya nchi ya Uturuki, endapo tu wale wote waliosafirishwa wataweza kupata ulinzi.
UNHCR inatoa mwito kwa viongozi wa Ulaya kuhakikisha mpango wake unajumuisha ulinzi sahihi wa kisheria kwa wakimbizi kabla ya kukutana wiki ijayo kukamilisha mpango wake na Uturuki.