Unesco, Rwanda zajadili vituo vipya vya Urithi wa Dunia

Watu wakijitolea kuzika mabaki ya wahanga wa mauaji ya halaiki ya mwaka 1994, Rwanda

Rwanda imeanza kuadhimisha Ijumaa kumbukumbu ya miaka 24 tangu kutokea mauaji ya halaiki yaliowauwa watu takriban millioni moja wengi wao wakiwa wa kabila la Watutsi.

Baraza la Seneti nchini Rwanda lilijadili Alhamisi suala la kutenga vituo vitatu vya kumbukumbu ya mauaji ya halaiki na kuvigeuza sehemu ya Urithi wa Dunia. Sherehe hizo zitaendelea kwa wiki nzima ambapo taifa zima linakuwa katika maombolezi na nyumba za starehe husitisha huduma zote ila zile za dharura.

Kwa mujibu wa gazeti la New Times, baraza la seneti limepokea ripoti ya mashauri ya kitaifa ya kupambana na mauaji ya halaiki inayoelezea hatua zilizofikiwa katika mazungumzo yaliyofanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO.

Mwenyekiti wa mashauri hayo ya kupiga vita mauaji ya halaiki, Damascene Bizimana aliliambia bazara la seneti kwamba kuna timu ya wajumbe wa UNESCO watakaoshiriki kwenye sherehe za maadhimisho ya wiki moja ya kumbukumbu ya mauaji ya halaiki, na wajumbe hao watazuru vituo hivyo vitatu ili kuvitathmini iwapo vinatimiza masharti yatakayo wezesha kugeuzwa kuwa sehemu ya urithi wa dunia.