Orodha hiyo ilipelekwa Alhamis kwa baraza la usalama kama sehemu ya ripoti ya kila mwaka ya Umoja wa Mataifa juu ya watoto katika maeneo yenye vita. Inasema ushirika unaoongozwa na Saudi Arabia uliwauwa au kuwajeruhi watoto 683 mwaka 2016 pamoja na kuthibitisha kufanyika mashambulizi ya anga 38 kwenye mashule na mahospitali.
Makundi mengine yanayopigana nchini Yemen ikijumuisha waasi wa kihouthi wanaoungwa mkono na Iran vikosi vya Yemen na al-Qaida katika peninsula ya kiarabu viliwekwa katika orodha tofauti kwa kushindwa kuwalinda watoto kutoka vitisho vya vita.
Lakini ripoti ilisema hatua zilizochukuliwa na ushirika wa Saudi Arabia zilipelekea watoto kuuwawa na kukatwa viungo hata kama Saudi Arabia inasema inachukua hatua kuepuka vifo vya mtoto. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema lengo la orodha hiyo ni kuhamasisha hatua ambazo zinaweza kutokomeza maafa yanayowakumba watoto katika mizozo.