UN yapinga uamuzi wa Marekani

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limekubali kwa pamoja azimio la kupinga uamuzi wa Marekani kuitambua Jerusalem kama makao makuu ya Israel na kitendo cha kuhamisha ubalozi wake huko.

“Marekani itaikumbuka siku ya leo ambayo ilishambuliwa peke yake katika Baraza Kuu kwa hatua yake ya kutumia haki yetu kama taifa huru," Balozi wa Marekani Nikki Haley ameuambia ukumbi uliokuwa umejaa kabla ya kupigwa kura.

“Tutaikumbuka siku hii pale tunapoitwa mara nyingine kutoa michango yetu mikubwa Umoja wa Mataifa, tutaikumbuka siku hii wakati nchi nyingi zikitutaka kuchangia zaidi, kama ilivyo kawaida, na kutumia uwezo tuliyokuwa nao kwa maslahi yao,” mwakilishi huyo aliongeza.

“Wale wanaounga mkono azimio la hivi leo ni kama vibaraka walioshawishiwa na mabwana wa vibaraka Wapalestina,” amesema Balozi wa Israeli Danny Danon.

“Nyie ni kama vikaragosi ambavyo hulazimishwa kucheza ngoma wakati uongozi wa Palestina ukiangalia kwa furaha."

Marekani na Israel ziliungwa mkono katika kura ya "hapana" na Guatemala, Honduras, Marshall Islands, Micronesia, Nauru, Togo na Palau. Pia zaidi ya nchi 20 hazikujitokeza katika kura hiyo ya utata.