UN yaionya Taliban ya Afghanistan kuhusu kudhibiti elimu kwa wanawake

Roza Otunbayeva, Mkuu wa Tume ya Misaada wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan

Mkuu wa Tume ya Misaada  wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan alitoa tena wito kwa utawala wa ki-imla kubadili vikwazo hivyo

Umoja wa Mataifa uliionya mamlaka ya Taliban ya Afghanistan leo Ijumaa kwamba marufuku yao ya elimu kwa wanawake pamoja na kufanya kazi inaisukuma zaidi nchi hiyo kwenye hatari ya umaskini mkubwa na kutengwa kimataifa.

Mkuu wa Tume ya Misaada wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan au UNAMA alitoa wito tena kwa utawala wa ki-imla kubadili vikwazo hivyo wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake inayomulika umuhimu wa kuwekeza kwa wanawake.

Inasikitisha kuona kwamba tunawaona mambo kinyume kabisa yakitokea nchini Afghanistan, janga na upotoshaji wa makusudi ambao unasababisha madhara makubwa kwa wanawake na wasichana, na kubuni vizuizi vya amani na ustawi endelevu, alisema Roza Otunbayeva.

Tangu ilipochukua madaraka hapo Agosti mwaka 2021, Taliban imewazuia wasichana kupata elimu ya sekondari na Zaidi ya hapo. Wamepunguza uhuru wa wanawake wa kutembea nje ya nyumba zao na kuwakataza wanawake wengi kufanya kazi katika sekta ya umma na ya kibinafsi, ikijumuisha Umoja wa Mataifa na makundi mengine ya misaada.