UN: Iran inawapa hifadhi viongozi wa kundi la Al-Qaeda

Wapiganaji wa kundi la Nusra Front, wenye ushirikiano na kundi la kigaidi la Al Qaeda

Marekani imesema kwamba inakubaliana na ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu mahali alipo kiongozi mpya wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price amesema kwamba Seif al-Adel anaishi nchini Iran.

Ned Prince amesema kwamba Iran inawapa hifadhi salama wapiganaji wa kundi la kigaidi la Al-Qaeda na kwamba nchi hiyo inaunga mkono ugaidi na kuendelea kuyumbisha utulivu katika Mashariki ya Kati na kwingineko.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inazingatia ujasusi wa nchi mwanachama, na ripoti hiyo inasema kwamba aliyekuwa afisa wa shughuli maalum za jeshi la Misri ndio sasa kiongozi mpya wa Al-Qaeda.

Seif al-Adel amekuwa kiongozi wa kundi hilo la kigaidi baada ya kuuawa kwa Ayman al-Zawahiri mnamo mwaka 2022, kutokana na shambulizi la kombora mjini Kabul, Afghanistan.

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amekanusha ripoti hiyo.