Shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu limesema linahitaji dola bilioni 2.6 kuwasaidia wale ambao bado wako ndani ya Sudan, likisema watu milioni 25 nchini humo wanahitaji misaada ya kibinadamu na ulinzi.
Ramesh Rajasingham, mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu mjini Geneva na pia ni mkurugenzi wa Kitengo cha Uratibu, alisema mapigano nchini Sudan yamekuwa ni "ukatili kwa watu wa Sudan."
Rajasingham alisema mzozo huo umesababisha vifo vya watu wasiopungua 676, na idadi halisi inawezekana kuwa mkubwa zaidi.
Dola nyingine milioni 400 zilizoombwa, zilitoka katika shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi ili kuwasaidia wale waliokimbilia nchi jirani wakiepuka mapigano nchini Sudan.
Mervat Shelbaya, mkuu wa tawi la misaada la shirika la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya uratibu wa masuala ya kibinadamu mjini Geneva, alisema katika kikao fupi siku ya Jumatano kuwa mapigano yamewalazimisha zaidi ya watu 950,000 kuyahama makazi yao na pia kuwalazimisha watu 220,000 kukimbilia nchi jirani.
"Ikiwa tunataka kuongeza mwitikio wetu na kuwafikia wale wote wanaohitaji, sisi na watu wa Sudan tunahitaji kuungwa mkono kwa kupewa msaada mkubwa na jumuiya ya kimataifa," Shelbaya alisema.
Baadhi ya taarifa za ripoti hii zilitoka kwenye shirika la habari la AFP na Reuters.