Umoja wa Mataifa wataka Darfur kuangaziwa ili kuleta amani

Umoja wa Mataifa, Jumamosi umetoa mwito wa kuchukuliwa hatua za haraka kukomesha mauaji ya kiholela ya watu wanaokimbia El Geneina, mji mkuu wa jimbo la Darfur Magharibi, na wanamgambo wa kiarabu wakisaidiwa na wanajeshi wa jeshi la taifa.

Kwa zaidi ya miezi miwili, jeshi la Sudan linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan limekuwa katika mapigano na kikosi cha dharura cha RSF kinachoongozwa na naibu wake wa zamani, Mohamed Hamdan Daglo.

Ghasia mbaya zaidi zimetokea Darfur, jimbo kubwa la magharibi kwenye mpaka na Chad ambapo Umoja wa Mataifa umeonya kuwa mzozo huo umechukua mwelekeo vita vya kikabila.

“Tuna wasiwasi mkubwa kwamba mauaji hayo ya kiholela yanaendelea na tunaomba hatua za haraka zichukuliwe,” msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani amesema katika taarifa.

“Watu wanaokimbia El Geneina lazima wahakikishiwe kupita salama na mashirika ya kibinadamu yaruhusiwe kuingia katika eneo hilo kukusanya miili ya waliouwawa,” aliongeza.