Umoja wa mataifa wasema wafanyakazi wake watano watekwa nyara Yemen

Walinzi wakisimama kwenye kifusi cha nyumba iliyoharibiwa na mashambulizi ya ndege za kijeshi yakiongozwa na Saudi Arabia, mjini Sanaa. Januari 18, 2022. Picha ya Reuters

Umoja wa mataifa ulisema Jumapili kwamba wafanyakazi wake watano walitekwa nyara kusini mwa Yemen.

Msemaji wa Umoja wa mataifa Eri Kaneko ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wafanyakazi hao watano walitekwa nyara katika mkoa wa kusini wa Abyan siku ya Ijumaa walipokuwa wakirejea kutoka katika mji wa bandari wa Aden, baada ya kukamilisha kazi zao.

“Umoja wa mataifa unawasiliana kwa karibu na maafisa wa Yemen ili wafanyakazi hao waachiliwe”, Kaneko ameongeza.

Haikufahamika mara moja ni nani aliyewateka nyara wafanyakazi hao wa Umoja wa mataifa.

Aden imekuwa makao makuu ya serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa baada ya kuondolewa katika mji mkuu Saana na waasi wa Kihuthi mwaka wa 2014.

Majeshi ya ushirika yanayoongozwa na Saudi Arabia yamekua yakiunga mkono serikali ya Yemen katika vita dhidi ya Wahuthi wanaoungwa mkono na Iran katika mgogoro uliosababisha vifo vya maelfu ya watu.

Mamilioni ya wengine walihama makazi yao katika kile Umoja wa mataifa umetaja mzozo mkubwa wa kibinadamu duniani.

.