“Kuna uwezekano mkubwa wa njaa kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu, na bila shaka baada ya kipindi hicho, ikiwa msaada wa kibinadamu hautaendelea kutolewa, na kama mvua za Aprili hadi Juni zitapungua kama inavyotabiriwa sasa,” Adam Abdelmoula, mwakilishi wa Umoja wa Mataifa na mratibu wa misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Somalia amewaambia waandishi wa habari.
Nchi hiyo, pamoja na maeneo mengine ya Pembe ya Afrika, yanakabiliwa na ukame wa kihistoria baada ya uhaba wa mvua kwa misimu mitano mfululizo.
Abdelmoula amesema karibu watu milioni 6.4 wanakabiliwa na viwango vya juu vya ukosefu wa usalama wa chakula na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi milioni 8.3 kati ya mwezi Aprili na Juni, ikiwemo watu 727,000 kati ya hao ambao wanatarajiwa kukabiliwa na viwango vibaya vya njaa.
Umoja wa Mataifa unasema wale walio katika hatari kubwa wako katika wilaya za Baidoa na Burhakaba na miongoni mwa waliokimbia makazi yao katika mji wa Baidoa na katika mkoa wa Bay na mjini Mogadishu.