Siku ya wakimbizi ya mwaka huu inaangazia hali mbaya ya wakimbizi milioni 35.4 na wanaotafuta hifadhi, juu ya mahitaji yao na haki za kisheria na usalama wao kote duniani.
Katika kuadhimisha siku hiyo, maafisa wa Umoja wa mataifa wanatoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti za kuboresha hali ya wakimbizi na jamii zinazowahifadhi.
Wanatetea pia suluhu ambazo zitawapa wakimbizi fursa ya kujijengea mustakabali mzuri wao wenyewe na wa familia zao.
“Niko hapa kuuambia ulimwengu wote kwamba tunaweza na lazima tuongeze juhudi ili kutoa matumaini, fursa na suluhu kwa wakimbizi, popote walipo,” amesema Filippo Grandi, Kamishna mkuu wa shirika la Umoja wa mataifa linalohudumia wakimbizi (UNHCR) katika maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani huko Kalobeyei, nchini Kenya.
Akizungumza kwenye hafla iliyofanyika katika kambi ya wakimbizi ya Kakuma, kambi kubwa duniani, Grandi ameipongeza serikali ya Kenya kwa mipango yake ya “kutekeleza sera bunifu na inayojumuisha watu wote.”