Ukurasa mpya wa makabiliano kati ya upinzani na serikali watarajiwa Kenya

Moses Wetangula, Spika wa bunge la kitaifa, Kenya.

Kubuniwa kwa Kamati ya kuratibu shughuli za Bunge na kuidhinishwa kwa Kamati ya Uteuzi ya Bunge la Kitaifa, pamoja na kuwekwa ratiba ya bunge hilo ya kuwapiga msasa watu 22 walioteuliwa kwenye Baraza la Mawaziri na rais William Ruto kunapelekea makabiliano.

Hali hiyo inafungua ukurasa mpya wa makabiliano kati ya Wabunge wa Upinzani na wabunge wa upande wa serikali.

Wabunge hao wa upinzani chini ya Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya unaongozwa na Raila Odinga wataonyesha upinzani kutokana na dukuduku iliyopo ya kimaadili kwa baadhi ya waliopendekezwa na Rais Ruto.

Wabunge hao wa Upinzani wakiongozwa na Kiongozi wa Walio Wachache bungeni humo Opiyo Wandayi, wameeleza kuwa hawawezi kutumika kama muhuri wa kupitisha baadhi ya waliopendekezwa kuwa mawaziri hata ingawa wana doa la kimaadili au wameshtakiwa kwa makosa yanayofungamana na uhalifu.

Shughuli hiyo ya upigiaji msasa mawaziri hao wateule, inayoanza Jumatatu wiki ijayo, inajiri baada ya bunge hilo kubuni Kamati ya kuratibu shughuli za Bunge inayotwikwa majukumu ya upangaji wa shughuli zitakazofanywa na Bunge na mambo yote yanayohusiana na Kanuni za Kudumu za bunge, baada ya kuwapo na sintofahamu iliyoonekana kusambaratisha uwezekano wa kutekeleza shughuli hizo.

Kamati hiyo ya wabunge 15 inayoongozwa na Spika wa bunge hilo Moses Wetang’ula, na kujumuisha naibu wake Glady’s Boss Shollei, Kiongozi wa Walio Wengi Kimani Ichungwa, naibu wake Owen Baya, Kiranja wa Walio Wengi Sylivanus Osoro na naibu wake Naomi Waqo pamoja na Kiongozi wa Walio Wachache Opiyo Wandayi, naibu wake Robert Mbui, Kiranja wa Walio Wachache Junet Mohamed na naibu wake Sabina Chege, inatakiwa kukamilisha shughuli ya kuwapigia msasa walioteuliwa kuwa mawaziri na kuwasilisha ripoti yake kwa bunge kabla Oktoba tarehe 27, kwa bunge hilo kuiidhinisha au kuipinga ripoti hiyo ifikapo Novemba 3.

James Gakuya, ambaye ni mbunge wa Embakasi Kaskazini chini ya Muungano wa Kenya Kwanza anaeleza kuwa Kamati hiyo itatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na wala haitapinga kwa sababu ya kupinga tu.

Muungano wa upinzani umewaelekeza wabunge wake kutokuwa sehemu ya upitishaji wa watu walio na shaka la kimaadili kuwa sehemu ya baraza la mawaziri.

Hata hivyo, Kimani Ichungwa ambaye ndiye Kiongozi wa Walio Wengi bungeni humo, ameeleza Alhamisi kuwa waliopendekezwa kuwa mawaziri wana kibarua kigumu cha kujieleza mbele ya kamati ya bunge na hakuna yeyote atakayeidhinishwa bila kuzingatia vigezo vyote vinavyohitajika kusimamia ofisi ya umma.

Kamati hiyo itahitajika kufanya mchakato wa uwazi, kwa kuzingatia sifa za kitaaluma za walioteuliwa, mafunzo ya kitaaluma na uzoefu, uadilifu binafsi na historia yao katika ofisi ambazo wamewahi kuzishikilia.

Wabunge, kisheria na taratibu za kudumu za bunge, wanatakiwa kuangazia vigezo alivyotumia rais kuufanya uteuzi wa afisa husika, matakwa yote ya kikatiba pamoja na wezo wa mtu aliyeteuliwa katika wadhifa, kwa kuzingatia iwapo uwezo, uzoefu na sifa zake zinakidhi kwa kiwango cha juu mahitaji ya ofisi ambayo ameteuliwa.

Ikiwa siku 28 zitakamilika kabla ya bunge kuzingatia uteuzi huo, kwa kuidhinishwa au kukataliwa, walioteuliwa wataidhinishwa kuwa mawaziri baada ya kula kiapo mbele ya rais, kwani sheria itakuwa inatekelezwa katika ombwe hilo.

Iwapo kutakuwa na waliokataliwa na bunge, ripoti itawasilishwa kwa rais, na atakuwa na nafasi ya kuwasilisha jina tofauti kwa uteuzi uliokataliwa chini ya utaratibu uliotumika awali.

Baada ya kupitishwa kwa ripoti ya walioteuliwa, karani wa bunge atamjulisha Rais kuhusu uamuzi wa Bunge ndani ya kipindi cha siku saba baada ya uamuzi huo, na hapo atakuwa na wajibu wa kushuhudia uapisho wao.

KENNEDY WANDERA, SAUTI YA AMERIKA, NAIROBI.