Ukraine yasema Russia ni taifa la kigaidi

Rais wa Russia Vladimir Putin alipotembelea Veliky Novgorod, Septemba 21, 2022

Wanajeshi wa Russia wameushambulia mji wa Ukraine kwa makombora, wakitumia ndege zisizokuwa na rubani zilizotengenezwa Iran.

Ofisi ya rais wa Ukraine imeyataja mashambulizi hayo manne kuwa tukio linalodhihirisha kwamba Russia imekata tamaa na inatekeleza mashambulizi kiholela, miezi minane baada ya kuanzisha vita ndani ya Ukraine na kuua maelfu ya watu.

Maafisa wa usalama wa Ukraine wameangusha na kuharibu ndege 37 zilizokuwa zimebeba makombora tangu Jumapili usiku.

Russia yaendelea na uvamizi Kyiv Ukraine March 21,2022

Mashambulizi hayo yametokea wiki moja baada ya mashambulizi kadhaa ya makombora katika mji mkuu wa Kyiv, na miji mingine kote nchini.

Majengo kadhaa yameharibiwa. Vitali Klitschenko ni meya wa Kyiv.

"Mashambulizi yameharibu miundo mbinu ya Ukraine na mji wetu. Wamesababisha watu kukaa bila joto nyumbani wakati huu wa baridi kali kutokana na ukosefu wa umeme. Russia inataka kusababisha janga la kibinadamu katika mji wetu na kuharibu majengo. Wameua watu katika mashambulizi yao dhidi ya majengo kadhaa.”