Ukraine yapuuza mapendekezo ya Russia

Majeshi ya Russia na vifaa vikiwa katika maeneo yanayotumika katika mashambulizi, kaskazini magharibi ya Uwanja wa ndege wa Antonov huko Lubyanka, Ukraine. Alhamisi, Machi 10, 2022. (Satellite image ©2022 Maxar Technologies via AP)

Ukraine imepuuza mapendekezo ya Russia ya kuigeuza kuwa nchi isiyoegemea upande wowote, huku Marekani ikijiandaa kutoa msaada mkubwa wa kijeshi kwa nchi hiyo.

Katika ardhi ya Ukraine, Makombora ya Russia yalishambulia kituo cha treni kusini nchini humo, kinachotumiwa na maelfu ya wakimbizi, huku milipuko mipya ikiulenga mji mkuu, Kyiv, ambako kumewekwa marufuku ya kutoka nje.

Hakuna majeruhi walioripotiwa, baada ya Russia kulipua madirisha katika kituo cha treni, kwenye mji wa Zapori-zizhia, ambako watu wamekuwa wakiwasili kutoka mji uliozingirwa wa Mariupol.

Mzozo huo tayari umepelekea zaidi ya raia milioni tatu wa Ukraine kukimbia makwao, kuvuka mipaka, na kuingia nchi jirani, wakati azimio la amani bado linaonekana kutoweza kufikiwa.

Mashambuzi zaidi dhidi ya Kyiv yalitarajiwa, ingawa kasi ya wanajeshi wa Russia ilionekana kupungua kutokana na upinzani kutoka kwa wanajeshi wa Ukraine, wanaotumia silaha za hali ya juu, za Magharibi.

Habari hii inatokana na vyanzo mbalimbali vya habari