Ukraine yapongeza vikwazo vya mataifa ya magharibi dhidi ya Rashia

Wanajeshi wa Ukraine wakitembea kwa mgu wakati wa mazoezi ya kijeshi karibu na mji wa Ukraine wa Kharkiv. Februari 10, 2022. Picha ya AP

Ukraine hii leo Jumatano imepongeza vikwazo mbali mbali vilivyowekewa Rashia na mataifa ya magharibi, hata hivyo kusema vikwazo zaidi vinahitajika ili kukabiliana na kitisho kinachoendelea kusababishwa na Moscow, mashariki ya nchi hiyo.

Wakati huo huo Bunge la nchi hiyo limepiga kura hii leo kupitisha mswada wa sheria ambao unaruhusu wanainchi wa Ukraine kumiliki silaha katika hali ya kujihami.

Nalo baraza la usalama la nchi hiyo limependekeza mswada wa kutangazwa hali ya dharura, ambao unahitaji kuidhinishwa na bunge.

Moja ya mizozo mibaya zaidi ya kiusalama barani Ulaya kwa miongo kadhaa umepamba moto baada ya rais wa Rashia Vladimir Putin kuyatambua rasmi majimbo mawili yanayotaka kujitenga huko mashariki mwa Ukraine, na kuamuru wanajeshi wa Rashia kuingia katika majimbo hayo.

Mzozo umeendelea kuwa mbaya baada rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine kusaini amri ya kuwataka baadhi ya wanajeshi wa akiba kujiunga na jeshi, akisema hii ni kutokana na mahitaji ya dharura ya jeshi la taifa.