Ukraine yapata Waziri Mpya wa Mambo ya Nje

Wabunge wa Ukraine, Alhamisi wamemteua Andriy Sybiga, mwanadiplomasia wa muda mrefu, kuwa waziri mpya wa mambo ya nje katika mabadiliko ya Rais Volodymyr Zelenskyy kwa washauri wake wakuu.

Sybiga, 49, anachukua nafasi ya Dmytro Kuleba, ambaye alikuwa na mchango mkubwa katika kushawishi washirika wa Magharibi wa Ukraine kuisaidia nchi yake kijeshi katika vita vya miezi 30 vya Ukraine dhidi ya uvamizi wa Russia.

Sybiga, ambaye anazungumza Kiingereza na Kipolishi, amekuwa naibu waziri wa mambo ya nje na pia aliwahi kuwa balozi nchini Uturuki.

Anaelezwa kuwa karibu na mkuu wa wafanyikazi wa Zelenskyy, Andriy Yermak, kuliko Kuleba, ambaye ndiye anayejulikana zaidi kutoka kwenye orodha ya maafisa wakuu wa Zelenskyy.

Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi jirani ya Poland, mshirika mkubwa wa Ukraine, ilimpongeza Sybiga kupitia mtandao wa X.