Ukraine inataka mazungumzo ya kweli na Russia

Rais wa Ukraine Zelenskiy akizungumza na waandishi wa habari mjini Kyiv, Ukraine, Sept 16, 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema kwamba yupo tayari kwa mazungumzo na Russia, lakini iwapo tu mazungumzo hayo yatakuwa ya kweli na yenye kuhakikisha kwamba Ukraine inarejeshewa mipaka yake na kuheshimiwa.

Mazungumzo hayo vile vile yanastahili kupatia Ukraine fidhia kutokana na mashambulizi ya Russia na kuwachukulia hatua kali wahusika katika uhalifu wa vita nchini humo.

Zelenskiy amesema hayo katika hotuba yake ya jumatatu usiku, siku moja baada ya gazeti la Washington post kuripoti kwamba Marekani inataka Ukraine kuonyesha dalili za kutaka mazungumzo yafanyike.

Washington post liliripoti kwamba hatua ya Marekani kutaka Ukraine kufanya mazungumzo na Russia ni ya kimkakati ili kuendelea kupata msaada kutoka kwa washirika wake.

Katika hotuba hiyo ambayo ameitoa kabla ya kuhutubia kongamano kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, Zelenskiy amesema kwamba mtu yeyote ambaye ana dhamira ya kweli kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, anastahili kuonyesha kwamba anajali sana kuhusu nia ya kukomesha vita vinavyoendelea Ukraine.