Ukraine inasema shambulio la kombora la Russia laua watu 3 mjini Kyiv

Jengo la makazi lililoharibiwa katika shambulio la kombora la Russia katika mji wa Chasiv Yar katika mkoa wa Donetsk nchini Ukraine, Mei 16, 2023.

Maafisa wa Ukraine Alhamisi wamesema shambulio la kombora la Russia limeulenga mji mkuu wa Ukraine, Kyiv na kuua watu watatu na kujeruhi wengine 10.

Jeshi la Ukraine limesema limezuia makombora yote 10 ya masafa mafupi yaliyorushwa na Russia.

Maafisa wa Kyiv wamesema mabaki ya makombora hayo yaliharibu majengo ya makazi, hospitali moja na bomba la maji.

Russia iliendesha mashambulizi kadhaa ya anga mwezi Mei wakati Ukraine ilikuwa ikijianda kufanya mashambulizi ili kudhibiti tena maeneo yaliyonyakuliwa na Russia tangu ianzishe uvamizi dhidi ya Ukraine mapema mwaka jana.

Gavana wa mkoa wa kaskazini mwa Russia wa Belgorod Alhamisi amesema shambulio la makombora ya usiku kucha yalijeruhi watu kadhaa katika mji wa Shebekino.

Gavana Vyacheslav Gladkov amesema kupitia mtandao wa Telegram kwamba shambulio hilo liliharibu pia majengo kadhaa, akiwatuhumu wanajeshi wa Ukraine kwa kufanya shambulio hilo.