Ukraine inapanga mkutano wa amani Februari mwakani

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa Baraza la usalama la Umoja wa mataifa juu ya hali nchini Ukraine, Septemba 22, 2022.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Jumatatu amesema kwamba serikali yake ina lengo la kuandaa mkutano wa amani mwishoni mwa mwezi Februari, pengine kwenye Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres inawezekana akawa mpatanishi, wakati wa maadhimisho ya vita vya Russia.

Lakini waziri wa Mambo ya Nje Dmytro Kuleba ameiambia Associated Press kwamba Russia itaalikwa tu kwenye mkutano huo ikiwa nchi hiyo itakabiliwa kwanza na mashtaka ya uhalifu wa vita mbele ya mahakama.

Kuleba amesema pia kwamba aliridhishwa sana na matokeo ya ziara ya Rais Volodymyr Zelenskiy hapa Marekani wiki iliyopita, na amefichua kuwa serikali ya Marekani imeandaa mpango maalum wa kufanya makombora ya kujihami ambayo ni msaada wa Marekani, yawe tayari kufanya kazi nchini Ukraine katika kipindi cha chini ya miezi sita.

Kuleba amesema katika mahojiano kwamba Ukraine itafanya lolote liwezekanalo kushinda vita mwaka ujao, akiongeza kuwa diplomasia kila mara ina mchango mkubwa.