Amnesty yatoa wito kufanyika mageuzi ya kweli Mashariki ya Kati

  • Sunday Shomari

Wapinzani wa utawala wa Syria wakionesha alama ya ushindi wakati wa maandamano huko Baba Amr katika jimbo la Homs.

Amnesty imesema serikali hazijatambua ukubwa wa mabadiliko wananchi wanataka na wale wanaodai mageuzi hawataweza kuzuiliwa.

Amnesty International inaeleza kwamba ukandamizaji na ghasia zitaendelea huko Mashariki ya kati hadi pale serikali katika kanda hiyo na mataifa makuu ya nje, yaamke na kukabiliana na kile wananchi wanachohitaji kwa kweli.

Katika ripoti iliyotolewa Junapili Amnesty imesema serikali hazijatambua ukubwa wa mabadiliko wananchi wanataka, na wale wanaodai mageuzi hawataweza kuzuiliwa kutokana na ghasia zinazofanywa na taifa.

Kaimu mkurugenzi wa Amnesty kwa ajili ya masuala ya Mashariki ya Kati Philip Luther anasema, "tunataka serikali kutambua kwamba kila kitu kimebadilika na ni wazi kwamba vuguvugu la waandamanaji kote mashariki ya kati na Afrika Kaskazini limeonesha bayana kwamba hawataweza kushawishiwa, hawataogoba vitisho katika kuendelea na vita vyao vya kupigania hadhi na haki.

Kwa sababu hiyo Luther anasema nchi za magharibi zinalazimika kuchukua tahadhari zinapowasiliana au kujadiliana na serikali zote mpya na za zamani katika kanda hasa kuhusiana na biashara ya silaha.

Amnesty pia inasema mataifa makuu ya kigeni yameshindwa kufahamu kiwango cha changamoto katika utawala wenye ukandamizi huko mashariki ya kati.

Inatambua uungaji mkono wakigeni uliotolewa kwa ajili ya upinzani wa wananchi huko Misri na Libya, lakini kukosoa ukosefu kabisa wa hatua ya kimataifa nchini Syria na Bahrain. Ripoti pia inataja majibu ya Umoja wa nchi za Kiarabu, Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya, hayawi sawa.

Luther alikosoa kile alichokieleza jukumu baya la Saudi Arabia na Iran na maamuzi ya Russia na China kuzuia kuchukuliwa hatua kali zaidi na Umoja wa Mataifa dhidi ya Syria.

Hata huko Tunisia ambako Amnesty ina uhusiano mzuri na rais mpya aliyewahi kuwa mfungwa wa kisiasa, kundi hilo linasema mageuzi hayafanyiki kwa haraka inavyohitajika.