Ujumbe wa Israel, unaongozwa na mkuu wa shirika la kijasusi la Israel la Mossad, David Barnea, upo Paris kwa mazungumzo yenye lengo la kuwarejesha mateka waliosalia wanaoshikiliwa na wanamgambo wa Kipalestina.
Wapatanishi wa amani mjini Paris wanafanya kazi Jumamosi ili kupatikana kwa sitisho la mapigano huko Gaza, kwa matumaini ya kuepusha mashambulizi ya Israel, kwenye mji wa kusini wa Gaza, wa Rafah, ambako zaidi ya watu milioni moja waliokimbia makazi wapo huko.
Vikosi vya Israel, vilianzisha mashambulizi zaidi ya 70 toka Ijumaa katika maeneo mbalimbali huko Gaza, ikiwa ni pamoja na Deir al-Balah, Khan Younis na Rafah.
Wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas, huko Gaza, Jumamosi imesema watu wasiopungua 92 wameuwawa katika mashambulizi hayo.
Israel, inasema itashambulia mji huo ikiwa hakuna makubaliano ya mapatano yatakayoafikiwa kwa sasa.