Ujumbe kutoka shirika la kimataifa la fedha IMF umetembelea Sri Lanka kwa mashauriano yanayolenga kuokoa uchumi wa taifa hilo lililotatizika na ambalo limebaki bila fedha za kigeni za kuagiza chakula , mafuta pamoja na dawa.
Mazungumzo hayo yameanza leo wakati shule na ofisi za serikali zikibaki kufungwa ili kupunguza matumizi ya bidhaa muhimu ambazo zimeendelea kudidimia. Kupitia taarifa, IMF imesema kwamba itaendelea kusaidia Sri Lanka katika kipindi hiki kigumu kuambatana na sera zake.
Timu hiyo ya watu 10 tayari imekutana na waziri mkuu Ranil Wickremesinghe wakati ikiendelea kubaki nchini humo kwa siku 10. Wachumi wanasema kwamba ziara hiyo ni muhimu ili kuokoa taifa hilo dhidi ya kufilisika. Mapema mwezi huu waziri mkuu aliambia bunge kwamba taifa hilo linahitaji takriban dola bilioni 5 ili kuweza kuagiza bidhaa muhimu katika miezi iliyobaki mwaka huu.