Ujumbe huo unaoongozwa na rais wa zamani wa Nigeria Abdulsalami Abubakar uliwasili katika mji mkuu wa Niger mapema Jumamosi alasiri, siku moja baada ya wakuu wa majeshi ya nchi wanachama wa ECOWAS kutangaza kwamba wako tayari kuingilia kati kijeshi kumrejesha madarakani rais aliyeondolewa.
Jumuia ya uchumi ya nchi za Afrika magharibi (ECOWAS) ilikubali kutumia “kikosi cha kuingilia kati muda wowote” kama hatua ya mwisho kurejesha demokrasia nchini Niger baada ya majenerali kumuondoa na kumuweka kizuizini Bazoum hapo tarehe 26 Julai. Lakini ilisema inaunga mkono mazungumzo ili kumaliza mzozo huo.
Ujumbe wa awali wa ECOWAS ulioongozwa na Abubakar Agosti 3 ulijaribu na haukufanikiwa kukutana na Bazoum na kiongozi wa mapinduzi, Jenerali Abdourahamane Tiani.
Chanzo kilicho karibu na ujumbe huo kimesema utatoa “ujumbe wa dhati” kwa maafisa wa kijeshi na kukutana na Bazoum.
Bazoum amezuiliwa na familia yake katika makazi rasmi ya rais tangu mapinduzi, huku wasiwasi wa jumuia ya kimataifa ukiongezeka juu ya hali yake ya kizuizini.