Ujumbe wa Baraza la Usalama la UM wamaliza ziara DRC

Ujumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Jumapili umekamilisha ziara yake ya siku tatu nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mabalozi waliokuwepo katika ziara hiyo waligusia suluhisho la kisiasa la kumaliza mgogoro wa kundi la M23.

Kundi hilo kwa sasa linashikilia maeneo kadhaa katika jimbo la Kivu Kaskazini toka liliporejea kufanya harakati zake mwaka 2021 baada ya kuwa kimya.

Wapiganaji wa M23 pia wamesonga mbele katika siku za karibuni, wakitishia kufunga barabara zote zinazo unganisha mji wa Goma, ambao una wakaazi zaidi ya milioni moja na unapakana na Rwanda.

Mapigano baina ya vikosi vya jeshi la serekali ya DRC, na M23 ambao wanashutumiwa kusaidiwa na Rwanda, yamesababisha kuwakosesha makazi watu zaidi ya 800,000 kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Ujumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa uliwasili Alhamisi, katika mji mkuu wa Kinshasa kabla ya kusafiri kwenda Goma, Jumamosi.

Mabalozi wa Baraza la Usalama watembelea kambi ya Bushangara karibu na Goma.