Shirika la taifa la upelelezi lakanusha taarifa za Trump kuwa hatarini

Mkurugenzi wa idaraya taifa ya upelelezi, James Clapper. Jan. 10, 2017.

Rais mteule, Donald Trump kwa hasira alikataa madai ya ripoti kwenye mkutano wake wa kwanza na wanahabari Jumatano.

Mkurugenzi wa idara ya taifa ya upelelezi Marekani, James Clapper amesema Jumatano kwamba alimueleza rais mteule, Donald Trump kwamba taasisi za kipelelezi hazikutengeneza nyaraka zilizo na madai kwamba Russia ilifanya udukuzi wa taarifa za kutaka kumweka Trump hatarini.

Baadhi ya mashirika ya habari yametoa taarifa zisizo na uthibitisho kamili Jumanne, lakini hawakutoa maelezo ya kina juu ya taarifa za nyaraka hizo zinazoweza kumweka rais mteule hatarini.

Lakini mtandao wa habari wa Buzzfeed umeweka kile walichodai kuwa Russia imekuwa ikimsaidia Trump kwa miaka kadhaa.

Katika taarifa yake James Clapper amesema idara za upelelezi za Marekani hazijafanya uamuzi wowote juu ya taarifa hizo kama ni za uhakika, na kwamba amemsisitizia Trump haamini taarifa hizo zilisambazwa kwa vyombo vya habari na vyanzo vya kipelelezi.

Donald Trump kwa hasira alikataa madai ya ripoti kwenye mkutano wake wa kwanza na wanahabari kama rais mteule Jumatano.

Wakati huo huo, msemaji wa rais wa Russia, Dmitry Peskov amesema kwamba madai hayo yana lengo la kuharibu uhusiano wa Marekani na Russia.