Uingereza na Ukraine zasaini makubaliano ya ushirikiano ya miaka 100

  • VOA News

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy na waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer wakizungumza kwenye mkutano huko Woodstock Uingereza, Julai 18, 2024. Picha ya Reuters

Uingereza na Ukraine Alhamisi zilisaini makubaliano ya miaka 100, huku Uingereza ikiahidi kuipa Ukraine msaada wa kijeshi wa dola bilioni 3.6 mwaka huu.

Makubaliano hayo yalitangazwa katika mkutano wao wa pamoja na waandishi wa habari mjini Kyiv kwenye Ikulu ambako waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer alijiunga na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy.

Starmer amefanya ziara yake ya kwanza nchini Ukraine tangu aingie madarakani.

Starmer aliyataja makubaliano hayo kuwa ya kihistoria na kusema ushirikiano huo mpya “unadhihirisha upendo mkubwa uliopo kati ya mataifa yetu mawili.”

Ushirikiano huo utajumuisha ushirikiano katika sekta za utamaduni, elimu, sayansi na teknolojia.

Kuhusu msaada wa kijeshi katika vita vyake dhidi ya Russia, starmer alisema Uingereza ina mpango wa kuipa Ukraine mkopo wa zaidi ya dola bilioni 2.6.

Alisema mkopo huo “hautolipwa na Ukraine, bali na riba kutoka kwenye mali za Russia zilizozuiliwa.”