Uingereza: Chama tawala chakumbwa na migawanyiko baada ya Boris Johnson kujiuzulu bungeni

Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Boris Johnson

Migawanyiko ya zamani imeibuka tena Jumamosi ndani ya chama tawala cha Uingereza cha Conservative baada ya waziri mkuu wa zamani Boris Johnson kujiuzulu ghafla katika bunge, huku chama cha upinzani cha Labor kikipata fursa nzuri kabla ya uchaguzi mkuu mwaka ujao.

Johnson amesitisha jana Ijumaa , shughuli zake za kisiasa alizokua anafanya kwa muda wa miaka 22 ili kulalamika dhidi ya uchunguzi wa wabunge kuhusu mwenendo wake alipokua waziri mkuu wakati wa janga la Covid 19, hasa pale alipofanya sherehe katika makazi yake ya Downing Street kwa kukiuka masharti makali ya kupambana na Covid.

Katika taarifa ya kujiuzulu, Johnson alikosoa vikali uchunguzi dhidi yake unaotaka kujua kama alipotosha bunge kuhusu sherehe hizo. Alimkemea pia waziri mkuu wa sasa Rishi Sunak.

Wabunge wa Chama cha Conservative watiifu kwa Johnson, baadhi yao ambao walipongezwa naye saa chache kabla ya kujiuzulu kwake, walisifu kazi yake kwenye mitandao ya kijamii.

Muda wa muhula wa utawala wake ulisitishwa kutokana na hasira katika chama chake na kote Uingereza juu ya kukiuka masharti ya kupambana na Covid kwa kufanya sherehe katika ofisi yake ya Downing Street ambayo ni makazi yake pia.

Johnson amesema kamati ya uchunguzi haikupata ushahidi hata mdogo dhidi yake.