Uingereza : Boris Johnson aongoza uchaguzi wa chama cha Konsavativ

Waziri mkuu mtarajiwa Boris Johnson

Boris Johnson amepata kura nyingi zaidi katika uchaguzi wa awali wa kumpata kiongozi wa chama cha Konsavativ na waziri mkuu atakaye mrithi Theresa May nchini Uingereza.

Wagombea watatu - Mark Harper, Andrea Leadsom na Esther McVey- wametolewa katika kinyang’anyiro hicho katika kura ya siri iliyopigwa katika Bunge la Uingereza.

Johnson alipata kura 114, Jeremy Hunt alifuatia kwa kupata kura 43 na Michael Gove alipata kura 37.

Wagombea saba wataingia katika mchuano wa raundi ya pili kupigiwa kura wiki ijayo.

Wabunge wawili maarufu zaidi watapelekwa mbele ya wajumbe wa Chama cha Conservative kupigiwa kura baadae mwezi huu.

Mshindi katika uchaguzi huo atamrithi Theresa May na anatarajiwa kutangazwa katika wiki ya Julai 22.

Johnson amesema “amefurahi kushinda duru ya kwanza ya uchaguzi, lakini ni safari ndefu mbele yetu”.

Waziri wa Mambo ya Nje Hunt amesema “ameridhika” kuchukuwa nafasi ya pili, akisema : Wakati huu muhimu unahitaji kiongozi aliyemakini.”

Na msemaji wa kampeni ya Michael Gove amesema : “ Kila mtu alikuwa ametubeza. Watu walikuwa wanasema tunarudi nyuma. Lakini tuliungwa mkono na hivi tunakaribia kumfikia aliyechukuwa nafasi ya pili. Hivyo kila mmoja ananafasi ya kushinda.”