Uingereza kupata waziri mkuu mpya wiki ijayo

Liz Truss mmoja wa wagombea wanaotarajiwa kuchukuwa wafidha wa waziri mkuu

Uingereza inatarajiwa kuwa na waziri mkuu mpya wiki ijayo karibu miezi miwili baada ya kujiuzulu kwa Boris Johnson mwezi Julai kufuatia mfululizo wa kashfa dhidi yake.

Wanachama wa chama cha konsavative watamchagua mrithi wake chancellor wa zamani Rishi Sunak au waziri wa sasa wa mambo ya nje Liz Truss ambaye kura ya maoni inaonyesha yuko mbele. Changamoto ya kwanza kwa atakayeibuka mshindi itakuwa ni vita vinavyoendelea Ukraine, wakati Uingereza ikiwa tayari imetoa takriban dola bilioni 2.7 kama msaada wa silaha kwa taifa hilo, tangu Russia ilipofanya uvamizi wake mwezi Februari.

Uingereza inachukua nafasi ya pili baada ya Marekani katika kutoa misaada kwa Ukraine. Mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka chuo cha King’s College mjini London Alan Wagner amesema kwamba Johnson alikuwa rafiki wa karibu wa Kyiv, na kwamba huenda mambo yakawa tofauti chini ya utawala wa Truss. Alan anasema kwamba huenda Truss akawekeza zaidi kwenye ulinzi wa taifa pamoja na kukuza uchumi.