Uhuru wa vyombo vya habari uko hatarini duniani kote, asema katibu mkuu wa UN

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres akitoa hotuba baada ya mkutano wa faragha kuhusu Afghanistan mjini Doha nchini Qatar, Mei 2, 2023.

Uhuru wa vyombo vya habari uko hatarini katika kila kona ya dunia, katibu mkuu wa Umoja wa mataifa alisema Jumanne, akilaani mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari na usambazaji wa habari za uongo.

Akizungumza siku moja kabla ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ambayo ni leo Jumatano, Antonio Guterres aliwasilisha malalamiko kwa niaba ya waandishi wa habari na vyombo vya habari kote ulimwenguni.

“Uhuru wetu wote unategemea uhuru wa vyombo vya habari,” alisema kupitia ujumbe wa video, akiutaja kuwa msingi wa demokrasia na haki” na uhai wa haki za binadamu.”

“Lakini katika kila kona ya dunia, uhuru wa vyombo vya habari uko hatarini,” Guterres aliongeza, akihutubia mkutano uliofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa mataifa mjini New York.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa hakutaja majina ya waandishi wa habari waliofungwa jela au kutoa lawama kwa nchi, lakini wazungumzaji wengine waliangazia kesi binafsi, kama ile ya mwandishi wa habari wa gazeti la Wall Street Journal Evan Gershkovich anayezuiliwa Russia kwa tuhuma za ujasusi, ambazo anakanusha.

“Vita vya uhuru wa vyombo vya habari, vita vya kuachiliwa kwa Evan ni vita vya uhuru wa kila mtu, mchapishaji wa Wall Street Journal Almar Latour aliliambia kongamano hilo.