Uhispania inapeleka wanajeshi 7,500 katika eneo lake la mashariki lililokumbwa na mafuriko makubwa, serikali ilisema Jumatatu wakati ikikabiliwa na ukosoaji mkubwa kuhusiana na jinsi inavyokabiliana na janga hilo, ambalo limesababisha vifo vya takriban watu 217.
Jeshi lilituma takriban wanajeshi 5,000 mwishoni mwa juma kusaidia kusambaza chakula na maji, kusafisha mitaa na kulinda maduka na mali, dhidi ya waporaji. “Wengine 2,500 wangejiunga nao,” Waziri wa Ulinzi Margarita Robles aliambia redio inayomilikiwa na serikali, RNE.
Meli ya kivita iliyokuwa imebeba maafisa wa jeshi la wanamaji wapatao 104, pamoja na malori yenye chakula na maji yalikuwa yakikaribia bandari ya Valencia, huku mvua kubwa ikiikumba Barcelona, takriban kilomita 300 kaskazini mwa Valencia.
Vikosi vya uokoaji siku ya Jumatatu vilikuwa vikitafuta miili katika maegesho ya chini ya majengo, ikiwa ni pamoja na maegesho ya magari 5,000 katika jumba la maduka la Bonaire karibu na uwanja wa ndege wa Valencia.